Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Katika khutuba yake ya kwanza, Sheikh Jalala alianza kwa kunukuu aya ya Mwenyezi Mungu isemayo:
{ إِنَّ عِدَّةَ ٱلشُّهُورِ عِندَ ٱللَّهِ ٱثنا عَشَرَ شَهۡرࣰا فِی كِتَـٰبِ ٱللَّهِ یومَ خَلَقَ ٱلسَّمَـٰوَ تِ وَٱلأرۡضَ مِنهَا أَرۡبَعَةٌ حُرُم...}
Hakika idadi ya miezi kwa Mwenyezi Mungu ni miezi kumi na mbili katika hukumu ya Mwenyezi Mungu tangu alipo umba mbingu na ardhi. Katika hiyo iko mine mitakatifu.
[Surah At-Tawbah: 36]
Akasema kwamba; maneno haya yanaashiria kuwa miezi hii ni ya amani, ambapo vurugu na machafuko havitakubaliwa. Sheikh huyo alisisitiza kuwa; kila Muislamu anapaswa kutumia muda huu kwa utulivu wa nafsi yake na jamii, huku akiimarisha uhusiano wake na Mwenyezi Mungu.
Aidha, Sheikh alielezea fadhila za mwezi wa Rajabu, huku akibainisha maneno ya riwaya yanayosema: "الا ان رجب شهر الله" Akasema kuwa; mwezi huu umepewa heshima maalum kwa sababu thawabu zake ni nyingi mno, na huruma za Mwenyezi Mungu huenea ndani yake. Rajabu ni mwezi unaotoa nafasi kwa kila mtu kufanya marekebisho ya nafsi, kutafakari maisha, na kuimarisha ibada.
Katika sehemu nyingine ya khutuba yake, Sheikh alisisitiza umuhimu wa kufunga na ibada nyingine ndani ya mwezi huu, huku akinukuu riwaya isemayo:
"الا فمن صام من رجب يوم استوجب رضوان الله الاكبر وابتعد عنه غضب الله واغلق عنه باب من ابواب النار"Mwenye kufunga siku moja katika mwezi wa Rajabu, zitampasa yeye radhi za Mwenyezi Mungu, na itamuepuka yeye ghadhabu ya Mwenyezi Mungu, na mlango wa motoni utafungwa kuepukana nae.
Alisema: Maneno haya yanaashiria thawabu kubwa kwa anayefunga mwezi wa Rajabu, funga hiyo ikimlinda dhidi ya hasira za Mwenyezi Mung. Sheikh alibainisha kuwa, fadhila hizi ni changamoto ya kiroho kwa waumini, na ni wito wa kuimarisha uhusiano wa mtu binafsi na Mwenyezi Mungu.
Pia, Sheikh alibainisha kuwa siku ya kwanza ya mwezi huu ni kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Imam Baaqir (as). Hii ni fursa ya kuyaenzi maisha na mafundisho yake, ambayo yamekuwa mwongozo kwa waumini katika utunzaji wa dini na maadili mema.
Sheikh alihimiza waumini wote kuutumia mwezi huu kwa kufanya ibada kwa moyo safi, kutafakari nafsi zao, na kueneza amani ndani ya jamii. Aliwashauri waumini wa Shia na wafuasi wa dini kwa ujumla kutoutumiaa muda huu kwenye mambo yasiyo ya lazima, bali kuutumia kuimarisha utu, huruma, na mshikamano wa kijamii.
Kwa ujumla, khutuba hii ilisisitiza kuwa mwezi ya Rajabu ni nafasi ya kipekee kwa waumini kufanya marekebisho ya kiroho, kutafakari maisha yao, na kupata thawabu kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Sheikh aliongeza kuwa kuenzi fadhila za mwezi huu ni njia ya kuimarisha amani, huruma, na upendo kwa waumini.
Maoni yako